Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini

Habari

SEKRETARIETI YA BARAZA LA LATRA CCC YATEMBELEA CLUB YA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI MIYUJI


Sekretarieti ya Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC), ikiongozwa na Katibu Mtendaji, Daud G. Daudi, imefanya ziara katika Shule ya Sekondari Miyuji, Jijini Dodoma, kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Club ya Wanafunzi, kujua hali ya uhai wake na kutathmini maendeleo yaliyofikiwa tangu kuanzishwa kwake.

Katika ziara hiyo, Sekretarieti ilipata nafasi ya kukutana na Mkuu wa Shule pamoja na Mwalimu Mlezi wa Club, ambapo walieleza mwenendo wa Club, shughuli mbalimbali zinazofanyika, ushiriki wa wanafunzi pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha Club inaendelea kuwa hai na yenye manufaa kwa wanafunzi.

Sehemu ya kuvutia katika ziara hiyo ilikuwa ni namna wanafunzi walivyotumia vipaji vyao vya ngonjera, nyimbo na maigizo kuwasilisha ujumbe wa elimu kuhusu masuala ya usafiri. Maonesho hayo yalionesha ubunifu, ujasiri na uwezo wa wanafunzi kutumia sanaa kama njia ya kujifunza na kuifikisha jamii ujumbe muhimu kuhusu usalama wa usafiri, haki za watumiaji na matumizi sahihi ya huduma za usafiri.

Kupitia ziara hii, Baraza limeendelea kutambua na kuhamasisha nafasi ya Club za Wanafunzi katika kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika masuala yanayowahusu kama watumiaji wa huduma za usafiri. Aidha, ufuatiliaji wa mara kwa mara unalenga kuhakikisha Club zinaendelea kuwa na shughuli, zinakua na zinafikia malengo yaliyokusudiwa.