Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini

Habari

TCF KUFANYA TAFITI KUWEZESHA TAIFA KUTUNGA SERA YA MLAJI(CONSUMER POLICY)


Jukwaa la watumiaji Tanzania limejipanga kikamilifu kukabiliana na changamoto mtambuka kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo ikiwemo kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tatifi zitakazowezesha taifa,kutunga sera ya mlaji(Consumer Policy),au kuboresha sera,sheria na kanuni zilizopo kwa lengo la kumlinda mlaji.

Leo Ngowi Mwenyekiti wa jukwaa la watumiaji Tanzania,lakini pia kaimu katibu mtendaji wa baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri ardhini amezungumza hayo jijini Mwanza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mtumiaji Duniani.

Ngowi amesema maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika Jijini Mwanza kwa lengo la kushiriki maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani yaliyoanza rasmi tarehe 14 Machi 2023,lakini pia ikiwa na kubadilishana uzoefu na kuendelea kujenga umoja na mshikamano wa Pamoja wa kuwakilisha na kulinda maslahi ya mtumiaji kwa sekta zinazodhibitiwa na zisizodhibitiwa.

Mwenyekiti huyo wa TCF amesema baada ya kufanya tafiti ndogo katika sekta zinazodhibitiwa na zisizodhibitiwa Jukwaa la watumiaji Tanzania limegundua changamoto mtambuka kama vile matumizi makubwa ya kuni na mkaa,kuongezeka kwa bei ya bidhaa za mafuta ya Petroli,Diesel na Mafuta ya taa,kukatika kwa umeme mara kwa mara kunakosababishwa na upungufu wa maji kwenye mabwawa,kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira.

Ameongeza pia changamoto nyingine kama vile watumiaji wa huduma kutokupata taarifa kwa wakati juu ya haki na wajibu wao kwenye nyanja mbalimbali,kuwepo kwa baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya mawasiliano kufanya uhalifu,kutokupata huduma stahiki kwa wakati na uwepo wa viashiria vya rushwa kwenye maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za jamii,udanganyifu katika bidhaa mbalimbali kama vipimo vya urefu,ujazo na uzito kupunguzwa bila mtumiaji kujua,maelezo ya bidhaa mbalimbali kuwa kwenye lugha ambayo mtumiaji haifahamu na vigezo na masharti yasiyo wazi kwa watumiaji.

Aidha Jukwaa la watumiaji Tanzania limejipanga kuendelea kumlinda mtumiaji dhidi ya mbinu zisizofaa za wafanyabiashara kujiongezea faida bila kujali maslahi ya mtumiaji,kuendelea kutoa Makala za Pamoja kwenye magazeti ya consumer voice,kuwafikia wadau mbalimbali kwa zaidi ya asilimia tisini na sita kwa kufahamu wajibu na haki zao katika sekta zote Nchini,ikiwemo kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita,inayoongozwa na Rais wetu Mh.Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kukabiliana na athari zitokanayo na mabadiliko ya tabia ya Nchi.

Akisoma hotuba ya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima,Mkuu wa Idara ya afya ofisi ya mkuu wa mkoa Dkt Thomas Rutha alianza kushukuru hatua ya Jukwaa la watumiaji Tanzania kuamua kuadhimisha siku ya mtumiaji Jijini Mwanza ''toka tarehe 13 Mei 2023 mmekuwa mkitoa elimu kuhusu shughuli zenu kwa wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari,vyuo vya elimu ya juu,wadau kutoka asasi za kiraia,viongozi wa serikali za mitaa na makundi mengine mbalimbali kwani elimu hiyo inawezesha mlaji kufahamu haki na wajibu wetu na kutujengea weledi katika kujisimamia na kujitetea tunapofanya manunuzi ya bidhaa na kulipia huduma kupitia fursa mbalimbali katika soko.

Dkt Rutha ameongeza kwa kusema kuwa kwa mujibu wa takwimu za wakala wa huduma za misitu Tanzania,zinaonyesha jumla ya ekari laki tatu elfu sabini na mbili mia nane na sabini na moja za miti hukatwa kila mwaka kwa ajili ya nishati ya kuni na mkaa na kwa hakika ukataji wa miti namna hii inahatarisha usalama wa mazingira na hivyo kuhitaji jitihada za haraka kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuelimisha umma wa watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi.''Kupitia wasilisho la shirika la petroleum Tanzania tumesikia kuwa Tanzania tunayobahati kubwa ya kuwa na gesi asilia,ambapo mpaka sasa gesi hii hutumika katika kuzalisha umeme,nishati ya kupashia joto kwa shughuli za uzalishaji viwandani,malighafi ya kuzalisha bidhaa mbalimbali za petrochemical na mbolea,Nishati ya kuendeshea magari na nishati ya kupikia hadi sasa nyumba elfu moja na mia tano kumi na moja na taasisi saba zimeunganishwa na haya ni mafanikio makubwa sana katika nchi yetu''.Alisema Dkt Rutha.

Maadhimisho ya siku ya mtumiaji Duniani yaliadhimishwa Jijini Mwanza kuanzia tarehe 13-15 Mei 2023 katika ukumbi wa Idara ya Maji,mgeni rasmi akiwa ni Dkt Thomas Rutha Mkuu wa Idara ya Afya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa akimwakilisha Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na mada ziliwasilishwa kwa mtumiaji kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Mamlaka ya Serikali Mtandao,Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT),kauli mbiu ikiwa ni ‘’kumjengea uwezo mtumiaji katika matumizi ya nishati na nishati mbadala’’.

Ikumbukwe kuwa mnamo Mwezi Mei 2010 viongozi wa FCC,FCT,NCAC,EWURA CCC,TCRA CCC,SUMATRA CCC hivi sasa LATRA CCC,TCAA CCC,FCC,FCT waliamua kwa Pamoja kukaa na kujadili juu ya utekelezaji wa majukumu yao na hatimaye kuona umuhimu wa kuwa na Jukwaa moja la kuunganisha nguvu ya kujadili na kuweka mikakati ya kutatua changamoto mtambuka,zinazowakabili watumiaji wa bidhaa na huduma mbalimbali Nchini.