Habari
FANYENI TAFITI ZINALIPA
Wanafunzi wanajukwaa la watumiaji wa huduma za usafiri ardhini chuo kikuu cha Dar es salaam wametakiwa kutumia fursa ya kufanya tafiti juu ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya mtumiaji kwani baraza linahitaji sana tafiti hizo zitakazosaidia kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya usafiri Nchini.
Akizungumza kwenye hafla ya kuwakaribisha wanajukwaa wapya wa UNIFORUM UDSM,Mwenyekiti wa jukwaa hilo Michael Matto amesema sekta ya usafiri inahitaji wasomi waje na masuluhisho ya matatizo mbalimbali hasa yanayohusu mtumiaji na sio kuendelea kulalamika.
"Nichukue nafasi hii kushukuru baraza kipekee Katibu Mtendaji,Wajumbe wa baraza na Sekretarieti kwa ujumla kuendelea kuwa walezi kwetu na kuhakikisha wanazidi kutusaidia kimalezi yaliyo bora kwetu kwakweli toka kuanzishwa kwa jukwaa hili tumekuwa tukipewa elimu na kupatiwa fursa mbalimbali kila zinapojitokeza ili kuimarishwa zaidi kwenye masuala haya ya kulinda maslahi ya mtumiaji na niombe tu,baraza msituchoke mzidi kutusaidia sisi kama wanafunzi ili baadae tuje kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya usafiri ardhini"alisema Matto.
Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza Leo Ngowi amesema kwa mujibu wa kifungu namba 31 (1)(e) kinatoa jukumu kwa baraza kuunda majukwaa kwenye maeneo ya shule,vyuo,taasisi zenye watumiaji wa huduma za usafiri wa sekta zinazodhibitiwa na kushauriana nazo,na jukumu hili limetekelezwa kwa kufungua jukwaa la UNIFORUM-UDSM na baraza linaendelea kufungua majukwaa mengine Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) na hivi karibuni baraza linampango wa kuzindua jukwaa lingine katika Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT)
Kwa upande wa wanajukwaa wapya waliokaribishwa wameomba baraza liwe na utaratibu wa kwenda kutoa elimu ya haki na wajibu kwa mtumiaji mara kwa mara kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza Changamoto zinazowakabili watumiaji wa huduma za usafiri ardhini Nchini.