Habari
SIKU YA HAKI ZA WATUMIAJI DUNIANI 2026
Mwenyekiti wa Jukwaa la Watumiaji (TCF) na Katibu wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC), Bw. Daud G. Daudi, akizungumza leo na waandishi wa habari, amesema Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa watumiaji ili kuhakikisha haki zao zinalindwa na kuchangia ustawi endelevu wa jamii.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Haki za Mtumiaji Duniani 2026, Bw. Daudi alieleza kuwa katika kuunga mkono kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Bidhaa Salama, Watumiaji Wenye Uhakika,” Mabaraza ya Ushauri ya Watumiaji (Consumer Consultative Councils – CCCs) yakiwemo LATRA CCC, EWURA CCC, TCAA CCC na TRA CCC yamepanga kutekeleza shughuli mbalimbali za kutoa elimu na uhamasishaji kwa watumiaji kuhusu haki na wajibu wao.
Aliongeza kuwa kupitia juhudi hizo, watumiaji watawezeshwa kufahamu haki na wajibu wao, kupata taarifa sahihi kuhusu huduma na bidhaa wanazotumia, pamoja na kuwasilisha malalamiko yao ili yashughulikiwe kwa wakati. Hatua hiyo itasaidia kuboresha ubora wa huduma na kulinda maslahi ya watumiaji.
Maadhimisho ya Siku ya Haki za Mtumiaji Duniani 2026 yanatarajiwa kufanyika tarehe 15 Machi 2026 katika viwanja vya Halmashauri ya Jiji la Tanga, yakibeba kaulimbiu isemayo “Bidhaa Salama, Watumiaji Wenye Uhakika.”

