Habari
WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI ARUSHA YANOGA.
WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI JIJINI ARUSHA YANOGA.
Imekuwa ni wiki yenye tija kubwa kwa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini kwakuwa waliweza kupatiwa elimu juu ya haki na wajibu wao watumiapo huduma za usafiri ikiwa ni pamoja na kufahamu majukumu ya baraza pamoja na utekelezaji wa majukumu hayo katika jamii.
Leo Ngowi Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri ardhini ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yaliyofanyika Jijini Arusha Kuanzia Novemba 23 2021 hadi November 27 2021 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Ngowi amesema kuwa baraza limekuja na mpango kabambe wa kutoa elimu kwa mtumiaji wa huduma za usafiri ardhini ikiwemo kukutana moja kwa moja na mtumiaji wa huduma za usafiri kwenye maonyesho mbalimbali ‘‘baraza limekuwa linahudhuria kwenye maonyesho mbalimbali lengo likiwa ni kukutana moja kwa moja na mtumiaji na kutoa elimu kwakuwa tunaamini hapa ni rahisi kuwafikishia elimu tofauti na maeneo mengine kwa mfano hapa uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwenye maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani tumewafikia watumiaji wengi na bado tunaendelea kukutana nao na kutoa elimu ya haki na wajibu wao wanapotumia vyombo vya usafiri na wengi wameshukuru kupatiwa elimu hiyo’’amesema Ngowi.
Kaimu Katibu huyo Mtendaji wa LATRA CCC ameongeza kwa kusema baraza ni chombo pekee kilichopewa jukumu kwa mujibu wa sheria kutetea maslahi mapana ya mtumiaji wa huduma za usafiri ardhini bado wanaendelea kupanua wigo wa utendaji kazi wa baraza kwa kuendelea kuimarisha na kuanzisha na kuratibu kamati za watumiaji wa huduma za usafiri katika mikoa mbalimbali ‘‘Kwasasa baraza linazidi kujiimarisha kwa kuanzisha kamati za watumiaji katika mikoa ambayo bado kulikuwa hakuna kamati ambapo hivi karibuni tumeshuhudia tumepata kamati mpya za watumiaji katika mikoa ya Kilimanjaro,Manyara,Lindi,Dodoma,Iringa,Ruvuma utaona kamati zote hizi zinakazi ya kuratibu,kushauri na kukusanya changamoto zinazowakabili watumiaji katika mikoa yao na kuziwasilisha baraza ambapo sasa baada ya kuzipokea tunazichaka hizo taarifa na kutoa ushauri wa kisekta’’aliongeza Ngowi.
Aidha baraza limeendelea kutoa elimu ya haki na wajibu kwa mtumiaji wa huduma za usafiri ardhini kwa kutumia mitandao mbalimbali ya kijamii ya baraza ambayo ni facebook,Instagram,Youtube,Twitter ambayo inapatikana kwa jina la LATRA CCC lakini pia kwenye tovuti ya baraza ambayo ni www.latraccc.go.tz, mtumiaji anaweza kuwasilisha maoni na changamoto zake moja kwa moja kwa njia ya barua pepe ya baraza, barua@latraccc.go.tz.
Lakini pia Leo Ngowi ameongeza kwa kusema kuwa elimu pia inatolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari lengo likiwa kumfikishia huyu mtumiaji elimu ya haki na wajibu wake ambapo ametaja baadhi ya haki za mtumiaji ikiwa ni haki ya usalama,haki ya kupata mahitaji muhimu,haki ya kupewa taarifa,haki ya kuchagua,haki ya kusikilizwa,haki ya kulipwa fidia,haki ya kusafiri katika mazingira salama,haki ya kuelimishwa na haki ya kugomea huduma au bidhaa zisizokidhi viwango.