Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini

Habari

WAZIRI KAMWELWE AZINDUA MFUMO WA TIKETI MTANDAO


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amezindua  mfumo wa Tiketi Mtandao unaotumika kukata tiketi za mabasi ya masafa marefu nchini huku akieleza kuwa  mfumo huo utaleta tija kwa Serikali,abiria,na wamiliki wa mabasi.

Akizungumza  mara  baada ya uzinduzi huo Mhandisi Kamwelwe alisema mfumo wa tiketi mtandao utaondoa upotevu wa mapato kwa wasafirishaji ambayo mara nyingi hupotelea katika mikono ya wapiga debe.

“Utawawezesha wasafirishaji kukopesheka kwa urahisi kwani taarifa za miamala yao zitaakisi moja kwa moja katika mabenki,pia utasaidia kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta kutokana na kuongezeka kwa mapato”alisema .

Mhandisi Kamwelwe alisema kwa upande wa abiria matumizi ya mtandao katika kununua tiketi utawaondolea abiria mlolongo wa kufunga safari kwenda vituo vya mabasi siku moja kabla ya safari waajili ya kukata tiketi.

“Pia utaondoa kero za abiria kubughudhiwa kwenye vituo vya mabasi na kufanya usafiri huu kuwa na heshima zaidi,utakomesha vitendo vya upandaji holela wa nauli hususan kipindi cha mwisho wa mwaka “alisema.

Alisema kwa upande wa Serikali mfumo huo utawezesha kupatikani kwa taarifa muhimu zenye kusaidia Serikali kufikia maamuzi sahihi kwakuwa ndio kitovu cha usafirishaji nchini.

“Mfumo huu utaisaidia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutambua idadi ya watu wanaosafiri kwenda maeneo mbali mbali hivyo itapanga huduma za usafiri kulingana na mahitaji ya eneo ya njia husika, mamlaka zinazohusika zitakuwa na uwezo wa kupanga sera za usafirishaji na ujenzi wa miundombinu kutambua maeneo ya kipaumbele ya usafirishaji”alisema .

Waziri Kamwelwe alisema mfumo huo utatumika kwa majaribio hadi kufikia Juni 2020 na baada ya hapo leseni haitotolewa kwa mmiliki ambaye hajajiunga na mfumo huu ili kuhakikisha kila mmiliki anatumia mfumo huu.

“Kufikia Septemba 2020 utekelezaji uanze kwa upande wa daladala nawaagiza kusimamia kanuni kikamilifu hususan mfumo huu kila atakaye kuja kuchukua leseni lazima aunganishwe na mfumo huu”alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu LATRA Gilliard Ngewe alisema kupitia mfumo huo watoa huduma hawatodanganywa tena kuhusu mapato yao kwani kila abiria anaponunua tiketi moja kwa moja hela ya mmiliki itakwenda benki na mwenyewe kupatiwa ujumbe kiasi cha pesa na idadi ya wateja watakao hudumiwa kwa siku .